1.0 Mwongozo wa Uzalishaji wa Mifugo , Nyama na Bidhaa za nyama
1.1 Mwongozo wa Ufugaji bora wa kibiashara
Mwongozo huu unalenga kuwapatia wafugaji elimu ya uzalishaji wa mifugo bora ikiwa ni malighafi za viwanda vya nyama ili kufikia uchumi wa kati na mapinduzi ya viwanda. Elimu hii itawalenga wadau ambao ni wafugaji/wazalishaji wa mifugo kwa lengo la kuzalisha nyama bora ya ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, punda, sungura na ndege wafugwao kwa lengo la biashara .Hivyo, wafugaji wataelimishwa kufuata kanuni bora za ufugaji ili kupata mazao yenye tija na kutumia fursa zilizopo ndani ya sekta ya mifugo
1.2 Ramani elekezi za machinjio na Mwongozo wa ujenzi na uendeshaji wa machinjio
Mwongozo huu utatumika pamoja na miongozo mingine (Mwongozo wa usafi wakati wa uzalishaji nyama na mwongozo wa madaraja ya ubora wa bucha) kutoa maelekezo kwa wadau na wawekezaji katika tasnia ya nyama ya kuboresha na kujengamiundombinu ya kuzalisha na kuuzia nyama bora na salama. Vilevile utajenga uelewa wa wadau kuhusu utaratibu wa kuzalisha na kuuza nyama kwa kuzingatia kanuni na taratibu zinazoelekezwa katika mwongozo huu. Ni matarajio yetu kuwa Mwongozo huu utazingatiwa wakati wa kukarabati na kujenga miundombinu hiyo ikiwa pamoja na kuzingatia taratibu za uendeshaji, uzalishaji na uuzaji wa nyama, kwa kufanya hivyo tutaweza kuongeza tija na ufanisi katika ukuaji wa tasnia ya nyama
1.3 Mwongozo wa taratibu za usafi katika uzalishaji wa nyama bora na salama (sops)
Mwongozo wa usafi katika uzalishaji wa nyama bora na salama umeandaliwa ili kutoa maelekezo kwa watendaji katika ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa ya kuzingatia wakati wa kusimamia usafi katika uzalishaji wa nyama kwenye hatua mbali mbali za mnyororo wa thamani.Pia wadau wa tasnia ya nyama watanufaika na mwongozo huu kwani umeandaliwa kwa lugha nyepesi na utawawezesha watumiaji kuelewa vizuri na kukidhi viwango vya ubora na usalama.
Mwongozo huu unatoa maelezo ya kanuni na taratibu zitakazotumika wakati wa uzalishaji wa nyama bora na salama kwa kuzingatia usafi katika mnyororo wa thamani, hususan uzalishaji wa awali, usafirishaji wa mifugo, maandalizi ya mifugo kabla ya kuchinjwa, hatua za uchinjaji, usafirishaji wa nyama, eneo, jengo, wafanyakazi na vifaa kwenye machinjio, viwanda na duka la nyama (bucha).
Ni matumaini ya Bodi ya Nyama Tanzania kwamba wadau na watendaji watazingatia mwongozo huu kikamilifu ili kufikia malengo tarajiwa na kusimamia ipasavyo Sheria ya Nyama Na. 10 ya Mwaka 2006 ili kuongeza ufanisi wa tasnia ya nyama na uchangiaji katika pato la Taifa kwa ujumla.
1.4 Mwongozo wa Madaraja ya ubora wa Bucha na uendeshaji wake
Mwongozo wa kuuza nyama na bidhaa zake umeandaliwa ili kuhakikisha biashara ya nyama inazingatia kanuni na taratibu za uzalishaji na hivyo kumpatia mlaji nyama bora na salama.
Mwongozo unatoa kanuni na taratibu za kuzingatia wakati wa kuendesha biashara ya nyama ikiwemo usajili wa duka la nyama, eneo linaloshauriwa kujenga duka la nyama, ramani ya jengo, vifaa, vyombo vinavyohitajika na usafi, uandaaji wa nyama na uuzaji. Vile vile mwongozo huu unaeleza kanuni za kuzingatiwa na wafanyakazi, wanunuzi na wasimamizi wakati wa kuuza nyama .
Matumizi ya mwongozo huu utawezesha watendaji katika maduka ya nyama kupunguza vichocheo vya vimelea vya vichafuzi vya nyama na hivyo kupunguza ubora na usalama wa nyama.