Watu binafsi na taasisi zinazotaka kutoa kitoweo cha nyama kama sadaka au qurban wametakiwa kabla ya kufanya hivyo kufika BAKWATA ili kuweza kupatiwa muongozo unaoelezea taratibu za kufuata katika utoaji wa sadaka na qurban.
Hayo yamesemwa na Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Bw. John Chasama alipokuwa akiongea na vyombo vya habari baada ya kikao cha kupitia rasimu ya tatu ya mwongozo katika uchinjaji wa wanyama kwa ajili ya sadaka na Qurban kilichofanyika Oktoba 25, 2024 jijini Dodoma.
Mbali na hayo, Bw. Chasama aliongeza kuwa wafanyabiashara ya nyama wanatakiwa wafuate taratibu za kufanya biashara hiyo na kuwasisitiza kufika Bodi ya Nyama Tanzania kupata ufafanuzi wa taratibu na kanuni zinazotakiwa kufuatwa badala ya kufanya biashara kiholela.
Bw. Chasama amesema “wafanyabishara za nyama wafuate taratibu na kanuni za biashara ya nyama na wafike ofisi za Bodi ya Nyama Tanzania ili kupata muongozo wa kanuni hizo”
Naye, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia afya ya jamii kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Stanford Ndibalema amesema kanuni za ukaguzi wa nyama zinataka mifugo ikaguliwe kabla ya kuchinjwa ila kutokana na kutokuwa na mwongozo huo taratibu hizo hazikuzingatiwa lakini sasa kwa kuwa kuna mwongozo taratibu hizo zitafuatwa kwani mwongozo umezingatia sheria za nchi na za dini ya kiislamu.
Dkt. Ndibalema ameongeza kuwa “nasisitiza wafanyabishara wafuate taratibu na kanuni kabla ya uchinjaji na uuzaji wa nyama ili kutoa kitoweo bora na jamii kununua nyama iliyokaguliwa na kuuzwa kwenye mabucha sahihi yaliyokaguliwa na Bodi ya Nyama Tanzania”
Vilevile, Mwakilishi Kutoka BAKWATA Bw. Husein Kuzungu amesema, BAKWATA imeichagua kampuni ya MIHB kusimamia masuala yote ya sadaka na qurban na watahakikisha muongozo huo unafuatwa.
Aidha, Bw. Mohamed Mitalo kutoka MIHB naye amesisistiza kuwa muongozo huo umezingatia afya za walaji na kuwalinda wafanyabishara ya nyama na kulinda maslahi yao kwani umezuia sadaka na qurban kuuzwa mabuchani na badala yake kugawiwa kwa walengwa husika.
Mwongozo huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa wataalam kutoka Bodi ya Nyama Tanzania, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwakilishi kutoka BAKWATA na Mwakilihsi kutoka kampuni ya MIHB iliyokasimishwa na BAKWATA kusimamia uchinjaji na wachinjaji nchini kwa mujibu wa taratibu za HALAL.