Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amewataka wafugaji na Wadau wa kuku nchini kuzingatia usalama wa chakula na sio kutafuta faida kubwa huku wakiangamiza taifa.
Mhe. Mnyeti ameyasema hayo wakati akifungua maonesho ya kuku na ndege wafugwao yanayofanyika kwa siku mbili kuanzia Oktoba 18, Mlimani city jijini Dar Es Salaam.
Mhe. Mnyeti amesema “ Natoa rai Wadau wote wa tasnia ya kuku kuhakikisha usalama wa chakula usitafute tu faida huku unaangamiza taifa lako kwa kuwalisha kuku chakula kisichofaa”.
Ameongeza kuwa “Usalama wa chakula mmekabidhiwa nyinyi wadau wa kuku kulinda afya ya mtumiaji wa mwisho”
Wakati huohuo katika kumlinda mtumiaji wa mwisho Mhe. Mnyeti amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe kupitia Taasisi ya Utafiti wa mifugo Tanzania (TALIRI) kupata taarifa za kutosha kuhusu madai ya baadhi ya wafugaji wa kuku kuwapa dawa aina ya ARV ili kuwakuza na kuwanenepesha, na ikibainika kuna ukweli wa taarifa hizo basi wahusika wachukuliwe hatua.
Vilevile Mhe. Mnyeti amewataka na kuwahimiza wadau wa kuku kufanya uwekezaji wa kimkakati ili kuinua tasnia hiyo na kukuza uchumi wa taifa.
Aidha, awali akimkaribisha mgeni rasmi Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema maonesho hayo yalitanguliwa na Jukwaa la tasnia ya kuku na ndege wafugwao kwa nchi za kusini mwa Afrika lililofanyika jijini Dar es Salaam lililoshirikisha wadau kutoka nchi 23.